CZRH YAENDELEA KUFANYA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MAGONJWA YA NJIA YA CHAKULA BILA UPASUAJI KWA KUTUMIA MASHINE YA ENDOSCOPY
Posted on: February 2nd, 2024Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) inaendelea kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa wanapata huduma za kibingwa na bingwa bobezi kutokana na uwepo wa wataalamu, vifaa na mashine za kisasa ambazo zimeletwa kupitia Serikali ya awamu ya Sita kwa lengo la kutatua changamoto za afya pamoja na kuokoa maisha ya wananchi.
Haya yamesemwa na Daktari Bingwa Bobezi katika masuala ya upasuaji Dkt.Brian C.Mawalla, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) mara baada ya kufanya uchunguzi (OGD) kwa wagonjwa ambao kati yao wamegundulika kuwa na uvimbaji wa mishipa ya damu ya koo na vidonda vya tumbo la chakula, hali ambayo ilipelekea kufika hospitalini hapa wakiwa wanatapika damu.
Dkt.Mawalla amesema, “matatizo haya mawili makubwa yanaweza kusababishwa na kichocho cha mfumo wa chakula, bakteria aina ya Helicobacter Pylori (H.Pylori), matumizi ya dawa za uvimbe(mfano aspirin), unywaji wa pombe kupita kiasi na kwa muda mrefu pamoja na uvutaji wa sigara.
Mwisho, Dkt.Mawalla ametoa wito na kuwakumbusha wananchi kuwahi kufanya uchunguzi na kupata matibabu mapema mara baada ya kuhisi dalili kama; maumivu ya juu ya tumbo, kiungulia, kubeua, tumbo kujaa gesi, kuhisi kuwaka moto tumboni, kichefuchefu na hata kupata kizunguzungu.Na ikiwa sababu ya vidonda haijatambuliwa na kutibiwa mapema dalili huweza kuendelea kwa miezi au miaka.Lakini kama utawahi na kupata tiba sahihi utaweza kupona na hakuna matatizo endelevu.
#Tunaboresha Huduma
#Tupo tayari kuokoa maisha.
#2024 “Uadilifu, Uvumbuzi,
Matibabu na Kujifunza”