Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe Martha Mkupasi akikabidhi nyumba mpya za watumishi wa hospitali ya rufaa ya kanda Chato
Posted on: June 30th, 2022Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Martha Mkupasi amekabidhi nyumba 20 zenye thamani ya shilingi milioni 860 kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Chato, ambapo ameutaka uongozi wa hospitali hii kuhakikisha wanaweka uzio katika nyumba hizi kwa ajili ya usalama wa watumishi.
"Nyumba hizi ni nzuri, tunatakiwa kuzitunza vizuri nyumba hizi pamoja na miundombinu yake ili ziweze kudumu" amesisitiza Mkuu wa Wilaya. Lakini Pia Mhe.Martha Mkupasi, amemuagiza Mwenyekiti wa kijiji cha Kitela kata ya Chato, Makoye Majani, kuitisha mikutano ya hadhara kwa lengo la kuzungumza na wananchi wanaozunguka makazi ya nyumba mpya za watumishi wa hospitali ya rufaa ya kanda Chato ili wawape ushirikiano mzuri watumishi hawa.
Mkurugenzi wa Hospitali Dk. Brian C. Mawalla ameishukuru serikali kupitia wizara ya Afya kwa kuendelea kuipatia fedha nyingi hospitali hii ambapo amesema kukamilika kwa nyumba hizo kutasaidia kutatua changamoto kubwa ikiwemo ya utoaji wa huduma za dharula ambapo hapo awali ilikuwa ni vigumu kuwapata watumishi kwa haraka. lakini pia kukamilika kwa nyumba hizi 20 ni mwanzo wa maandalizi ya ujenzi wa nyumba zingine 20 ambapo amesema tayari wameomba fedha. Ameongeza kusema watumishi waliopewa kipaumbele kwenye nyumba ni wale wanaotoa huduma za dharula hospitalini hapa.
"Mbali na kuishukuru serikali nyumba hizi zitasaidia kuinua hali ya utendaji kazi kwa watumishi ambao sasa tutaishi jirani kabisa na hospitali hii ya rufaa ya kanda Chato na itaturahisishia kufika hospitalini hapa kwa wakati"amesema Dk. Matoke Muyenjwa
