MRADI WA UZALISHAJI HEWA TIBA YA OKSIJENI (OXYGEN PLANT) WAKAMILIKA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO.
Posted on: December 19th, 2023Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato imeanza kutoa huduma ya uzalishaji wa hewa tiba ya Oksijeni (Oxygen Plant), hii ni mara baada ya kukamilika kwake. Mradi huu ni juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo, kupitia Wizara ya Afya, Serikali imeendelea kuboresha utoaji huduma za afya na sasa hospitali imekamilisha usimikaji wa mitambo ya uzalishaji wa hewa tiba ambayo itasaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wake pamoja na gharama kubwa ambazo hapo awali zilitumika kufuata huduma hii mbali kwa ajili ya wagonjwa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi huu, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, Dkt. Brian C. Mawalla amesema “Tunaishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya inayoongozwa na Waziri Mhe. Ummy Mwalimu ambayo imeendelea kuhakikisha hapo mbeleni hospitali hii inajitegemea katika utoaji wa huduma za afya kwani hadi sasa tumepokea mitambo ya kisasa ya uchunguzi kama MRI, CT Scan, mashine ya kisasa inayotumia hadubini kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na mfumo wa hewa na mitambo mingine ambayo imekuwa chanzo cha ukuaji na kuongezeka kwa huduma katika hospitali hii ukilinganisha na hapo mwanzo.”
Dkt. Mawalla ameendelea na kusema; “ mtambo huu wa uzalishaji hewa tiba umekamilika na una uwezo wa kuzalisha mitungi kumi (10) kwa saa moja ambapo kwa siku unazalisha mitungi miambili arobaini (240). Lakini pia mtambo huu umeunganishwa moja kwa moja kuelekea katika jengo la wodi na utakuwa ukipeleka hewa tiba hii hadi alipo mgonjwa ndani ya wodi mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa jengo hili.”
Mwisho, Dkt. Mawalla ametoa rai na wito kwa hospitali na vituo vya afya vilivyopo kanda ya ziwa kuitumia fursa hii ambayo itawasaidia kupunguza adha ya usumbufu na gharama kubwa kuifuata huduma hii mbali kama ilivyokuwa hapo awali, na hivyo kuelekeza gharama hizo katika kuboresha huduma nyingine za afya.