KUELEKEA MWAKA MMOJA WA MAFANIKIO- HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA YA CHATO

Posted on: July 27th, 2022

Leo kwenye ufunguzi wa juma la maadhimisho ya mwaka mmoja wa utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda- Chato ambayo ilianza kutoa huduma za rufaa tarehe 30 Julai 2021, Mkuu wa Wilaya ya Chato Martha Mkupasi ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya hii na maeneo jirani na mkoa wa Geita kwenda kupatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Kanda Chato iliyopo wilayani Chato kwani kwa sasa hospitali inavifaa vya kutosha na inatoa huduma za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali. Mkuu wa Wilaya ya Chato amesema “Kwa sasa hospitali ina wataalamu wengi waliobobea, ina vifaa vingi na vizuri leo tumejionea wenyewe ndani ya hospitali hii, ni Imani yangu wagonjwa watatibiwa vizuri na kwa wakati”.

Mbunge  wa jimbo   la Chato  Dkt. Medard  Kalemani  ameishukuru  serikali  ya  awamu  ya sita kuendelea kutoa fedha kukamilisha ujenzi wa hospitali hii ambapo amesema kukamilika kwa hospitali ya Rufaa ya Kanda  Chato imesaidia wananchi wa Chato na mkoa wa Geita kwa ujumla kupatiwa matibabu kwa gharama nafuu na haraka.

“Mheshimiwa Rais atembee kifua mbele, fedha anazoleta tunaona zinafanya kazi nzuri, na sisi tunamhakikishia   tutalinda   miundo mbinu   ya   hospitali   hii   kwani   matunda   yake   tunayaona” amesema Mhe. Dkt. Medard Kalemani

Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Chato Dkt. Oswald Lyapa amesema tangu   hospitali ianze kutoa huduma   tarehe 30 Julai   2021, imeweza kuhudumia   wagonjwa 10,502  wanaotoka mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma na Shinyanga. 

Akisoma risala kwenye ufunguzi wa wiki ya huduma kwa wateja inayolenga kutoa matibabu ya kawaida na yale ya kibingwa bure kwa wagonjwa mbali mbali,kaimu mganga mkuu wa hosptali hiyo, Dk. Osward Lyapa, amesema uwepo wa hospitali hiyo imekuwa ni faraja kubwa sana kwa jamii baada ya huduma za magonjwa makubwa kupatikana umbari mfupi ikilinganishwa na iwapo wagonjwa wangepelekwa hospitali ya Jakaya Kikwete jijini Dar es salaam.

Mtaalamu wa huduma za mionzi kwenye hospitali hii, Magesa Mokiri, amedai mpaka sasa wagonjwa wa moyo 50 wamepokelewa na kupatiwa huduma za kibingwa na kwamba jamii imeanza kutambua thamani ya uwepo wa hospitali hii,lakini ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kutatua changamoto ya uhaba wa wataalamu wa tasnia ya mionzi kutokana na waliopo sasa kuwa watatu licha ya mahitaji kuwa ni watumishi 8.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.