UFUNGUZI WA KAMBI MAALUMU YA SIKU TANO ZA UCHUNGUZI NA MATIBABU BURE KUTOKA KWA MADAKTARI BINGWA WA CZRH WILAYA NYANG'HWALE

Posted on: October 30th, 2023

Wananchi wa wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita, wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika hospitali ya wilaya hiyo ndani ya siku tano za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya wanawake na uzazi, magonjwa ya watoto, magonjwa ya ndani na yasiyoambukizwa, matibabu ya mifupa na viungo pamoja na upasuaji wa jumla ambapo Madaktari Bingwa kutoka hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato wanatoa huduma hizi bure kuanzia leo 30 oktoba hadi 4 Novemba, 2023.

Wito huu umetolewa na kaimu Katibu Tawala mkoa wa Geita Bi. Kaunga Omary Amani wakati akizungumza na wananchi mapema leo katika ufunguzi wa kambi ya utoaji huduma hizi akisema, "Nimefarijika na nipende kuchukua nafasi hii kuwapongeza na kumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, Dkt. Brian Mawalla pamoja na madaktari na wataalamu hawa kukubali ombi hili la kutimiza dhamira ya dhati ya Rais wetu Mhe.Dkt.@samia_suluhu_hassan ambaye yeye ameonesha nia ya kuhakikisha huduma za afya zinamfikia kila mtanzania popote alipo. Niwashukuru hospitali hii kwa utekelezaji wa dhamira hii kwani bila nyie leo, sidhani kama mkutano huu ungekuwa na watu kiasi hiki.Wananchi wa Nyang'hwale tumepata neema hii nitoe wito tukaitumie na mimi kwa vifaa hivi nilivyoviona vya kisasa naahidi nitatibiwa hapahapa".

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nyang'hwale Bi. Husna Toni hakusita kutoa shukrani kwa mwitikio wa wananchi waliofika kupata huduma hizi za kibingwa huku akiwasihi kuwaeleza wataalamu hawa matatizo yote ya kiafya yanayowasumbua kwani ni fursa ambayo haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa wilaya hii mwaka 2012/2013 ambapo huduma za afya zilikuwa zikitolewa chache sana.

Aidha, mwakilishi wa madaktari bingwa na wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya watoto, Dkt. Gerald Muniko ametoa wito kwa wananchi kuitumia fursa hii ya siku tano kufanyiwa uchunguzi na matibabu haya kwani ni mpango wa serikali yetu kupitia @wizara_afyatz chini ya Waziri Mhe.@ummymwalimu, kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na huduma za kibingwa nchi nzima; huku tukitoa elimu namna bora ya kujikinga na magonjwa mbalimbali hasa yale yasiyoambukizwa.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.