WATUMISHI WA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO (CZRH) WAPATA MAFUNZO YA MATUMIZI YA MIFUMO YA KIUTUMISHI KATIKA KUBORESHA UTENDAJI KAZI.

Posted on: January 17th, 2024

Wakuu wa idara,vitengo na watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) leo Januari 17, 2024, wamepokea mafunzo ya matumizi ya mifumo ya utumishi (PEPMIS) yenye lengo la upimaji utendaji kazi wa kila mtumishi wa umma na taasisi.

Mafunzo haya yameendeshwa na Maafisa kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambao ni Bi. Maryam S. Mloly na Bwana. Royald S. Matiko ambao wamesisitiza matumizi ya mifumo ya TEHAMA ambayo inaenda kutatua changamoto za kiutendaji kazi kwa watumishi na taasisi kwa ujumla.

Aidha Bwn.Royald amesema, mafunzo ya mifumo hii yanalenga kuwaongezea watumishi wa umma ujuzi na ari ya kuitumia mifumo ya TEHAMA ambayo imebuniwa ili kuboresha utendaji kazi serikalini na kumpima mtumishi mmoja mmoja ambapo mwajiri atakuwa na uwezo wa kuona namna watumishi wake wanavyofanya kazi zao za kila siku.

Naye Bi. Maryam ameongeza na kusema “kupitia mifumo hii ya kiutumishi hakutakuwa tena na mfumo wa zamani (OPRAS) ambao ulionekana kushindwa kupima uhalisia wa kiutendaji kwa watumishi na sasa kila mmoja atawajibika na kujituma kila siku katika Kuhakikisha anawatumikia wananchi kwa weledi.

Mwisho, wakufunzi hawa wameushukuru uongozi na watumishi kwa mapokezi mazuri na kuonesha utayari wa kujifunza matumizi ya mfumo huu huku Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato DKt. Brian C. Mawalla akihitimisha mafunzo haya kwa kuishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais DKt. @samia_suluhu_hassan kubuni mifumo hii ambayo inaenda kuongeza hali ya uwajibikaji na ufanyaji kazi kwa umahiri ambayo italeta ufanisi wa kiutendaji na kuzingatia haki na wajibu wa kila mtumishi.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.