Public Health Education

Ijue Saratani ya Shingo ya Kizazi

SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI  NI NINI?

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ambayo hutokana na mabadiliko ya mfumo wa chembechembe au cells zilizoko katika shingo ya kizazi. Mabadiliko haya hupelekea chembe chembe hizo kushamiri na kuzaliana kwa kasi kinyume na mpangilio wa maumbile.Saratani ya Shingo ya kizazi yasemekana kuwa ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea. Ripoti ya 2012 ya shirika la afya duniani 'WHO' imesema kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya kizazi barani Afrika, 50,000 walifariki dunia. 

NINI KINACHOSABISHA SARATANI YA SHINGO YA UZAZI?

Ripoti za utafiti wa kisayansi zimeafiki kuwa asilimia 99% ya saratani za shingo ya kizazi hutokana na maambukizi ya virusi vya 'Human Papillomavirus' au HPV vilivyoko katika jamii ya papilloma. Baadhi ya virusi hivi vyenye aina zaidi ya mia moja huambukizwa kwa njia ya kujamiana.

BAADHI YA MAMBO YANAYOONGEZA HATARI ZA KUPATA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

  • Kushiriki tendo ndoa katika umri mdogo au chini ya miaka 18. 
  • Kuwa na wenzi tofauti au mwenzi aliye na wapenzi tofauti.
  • Utumiaji wa sigara kwani hupunguza nguvu ya kinga mwilini(impairs immune system).
  • Watu wenye kinga hafifu ya mwili au magojwa kama Ukimwi.
  • Uzazi wa mara kwa mara

BAADHI YA DALILI ZA SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

  • Kutokwa na majimaji au uchafu wenye harufu kali ukeni.
  • Kutokwa na damu ukeni mbali na siku za mwezi au baada ya tendo la ndoa.
  • Maumivu makali ya sehemu ya chini ya tumbo ( pelvic area).
  • Kuhisi maumivu makali wakati wa kujamiiana.
  • Kupungua kwa uzito wa mwili bila kukusudia.
  • Mkojo wenye matone ya damu

JE SARATANI YA SHINGO YA KIZAZI HUTIBIKA?

Saratani ya shingo ya kizazi yaweza kutibika iwapo itagundulika mapema. PAP TEST (PAPANICOLAOUS TEST);Pap-Smear ni kipimo ambacho hutumika kuchunguza mabadiliko ya chembe zilizoko katika mlango wa kizazi ili kugundua mabadiliko yanayotokea katika chembe hizo na hivyo kuwahi kuyakabili mapema.

UMRI WA KUPATA PAP TEST

Test hii hushauriwa kwa wanamke wa umri wa miaka 21 hadi 65 na chini ya umri wa miaka 21 endapo ameingia katika tendo la ndoa kwa kipindi kisichopungua miaka 3. 

KUPUNGUZA HATARI ZASARATANI YA SHINGO YA KIZAZI

  • Pap tests.

 Waweza kupata Pap test mara 1 kwa mwaka au mara 1 kwa miaka 2- 3,hii itategemea ushauri wa daktari,umri,hali yako ya afya kwa ujumla, na majibu uliyoyapata katika testi zilizotangulia na mfumo    wako wa maisha. 

  • Pata HPV vaccine (hii yashauriwa kati ya umri wa miaka 12 hadi 26 chini ya mwongozo wa daktari) . 
  • Kuwa na mpenzi mmoja. 

           Mahusiano ya kimwili na mtu mmoja hupunguza hatari za maambukizi ya magojwa ya zinaa. 

  • Tumia kinga (condoms). Hii husaidia kupunguza maambukizi ya magojwa ya zinaa.
read more
Mpango Binafsi wa kujifungua Salama

 ANDAA,ZUNGUMZA NA MWENZI WAKO,JAZA MPANGO

  • Fahamu tarehe ya kujifungua.
  • Fahamu na uhakikishe kituo cha kutolea huduma za afya au hospitali utakapojifungulia.
  • Fanya mpango wa usafiri wa kukufikisha mapema kwenye kituo cha kutolea huduma za afya utakapojifungulia.
  • Nani atakaye kusindikiza kwenye kituo cha kutolea huduma za afya mapema ili ujifungulie huko.
  • Tayarisha mfuko utakapoweka nguo za mtoto na mahitaji yote wakati ukiwa katika kituo cha kutolea huduma za afya.
  • Nani utakayemwachia nyumba utakapoenda kujifungua?
  •  Jadili na mwenza wako na mtoa huduma iwapo unataka kubadili mpango

ORODHA YA HUDUMA KWA MAMA MJAMZITO UENDAPO KLINIKI

  • Vipimo vya kuzingatia kila uendapo kliniki
  • Kipimo cha presha ya damu
  • Kipimo cha kiwango cha damu
  • Kipimo cha mkojo
  • Mtoto anavyoendelea kukua tumboni
  • Vipimo vinavyofanyika angalau mara moja wakati wa ujauzito
  • Kipimo cha kundi la damu
  • Kipimo cha magonjwa ya zinaa mfano Kaswende
  • Kipimo cha Virusi Vya Ukimwi kwako na mwenza wako(kawaida mara mbili)
  • Hakikisha unapata vitu hivi
  • Chandarua chenye dawa( viatilifu)
  • Chanjo za pepopunda
  • Vidonge vya kuongeza damu(Tumia kila siku wakati wa ujauzito na endelea kutumia vidonge vya kuongeza damu mpaka miezi mitatu baada ya kujifungua)
  • Dawa za minyoo(Tumia mara moja baada ya miezi mitatu ya ujauzito
  • Vidonge vya SP kuanzia wiki ya 14 ya ujauzito na kila unapohudhuria kituo cha kutolea huduma za afya.

DALILI ZA HATARI KABLA YA KUJIFUNGUA/WAKATI WA KUJIFUNGUA/BAADA YA KUJIFUNGUA

  • Uonapo dalili hizi nenda kituo cha kutolea huduma za afya mara moja!!!
  • Kutoka damu ukeni
  • Kuumwa sana na kichwa na kuona maluweluwe/kushindwa kuona
  • Kupoteza fahamu au mtukutiko mwili/kifafa cha mimba
  • Kuchoka haraka ,kupumua kwa shida
  • Homa
  • Mtoto kuacha au kupunguza kucheza tumboni.
  • Dalili za ishara za uchungu wa kujifungua
  • Mkazo na kuachia kwa misuli ya mfuko wa uzazi unaoendelea kuongezeka na kusababisha  maumivu makali ya tumbo na kiuno hadi kujifungua.
  • Kutokwa mchozo ute wenye damu.

KUMBUKA: Kama unaishi mbali na kituo cha kutolea huduma za afya ,ni busara kuhamia kwa muda karibu na kituo hicho,kadiri siku ya kujifungua inavyokaribia.


Imeandaliwa na:

DOROTHY A LEMA

MRATIBU WA HUDUMA YA AFYA YA UZAZI NA MTOTO -TANGA


read more
Ijue Saratani ya Kinywa

SARATANI YA KINYWA

Saratani ya kinywa ni ile saratani ambayo inatokea katika maeneo mbalimbali ya kinywa. Hivyo saratani hii huweza kutokea kwenye maeneo kama vile:

  • Midomo
  • Fizi
  • Ulimi
  • Sehemu za ndani za kinywa
  • Kaakaa
  • Sehemu ya kinywa iliyo chini ya ulimi

Saratani zinazotokea kinywani ni mojawapo ya saratani zilizomo katika makundi ya saratani zinazoathiri maeneo ya shingo na kichwa, na hata matibabu yake huwa sawa kwa kiwango fulani.

DALILI ZAKE

  • Dalili na alama za saratani ya kinywa huweza kuwa zifuatazo:
  • Kidonda kisichopona
  • Kidonda ambacho kinatoa damu kikiguswa kidogo tu
  • Kuota kwa kitu kipya kinywani, ama uvimbe katika sehemu yeyote ya kinywa
  • Maumivu makali ya ulimi
  • Kushindwa kutafuna ama kuwa na maumivu wakati wa kutafuna
  • Kuwa na maumivu wakati wa kumeza chakula

NI WAKATI GANI UMUONE DAKTARI

Ni vizuri kumuona daktari mara tu uonapo mojawapo ya dalili hizo kinywani ambazo zipo kwa zaidi ya wiki mbili. Daktari ataweza kufanya uchunguzi kulingana na dalili zake, na pia kumuwezesha daktari kutofautisha kati ya maambukizi yanayoweza kuwa na dalili kama hizo wakati si saratani.

SABABU ZA KUTOKEA KWA SARATANI 

Saratani kwenye kinywa hutokea wakati chembe hai(cell) zilizoko kinywani na maeneo yote ya kinywa  zinapopata mabadiliko kwenye vinasaba vyake (DNA). Mabadiliko haya husababisha chembe hai hizi kuzaliana na kukua nje ya utaratibu na wakati huohuo chembe hai zilizo na afya kufa. Ni mkusanyiko huu wa chembe hai ndio unapelekea kutokea kwa saratani husika. Kadiri muda unavyokwenda ndivyo ambavyo saratani huweza kusambaa katika maeneo mengine ya mwili kama vile shingoni, n.k.

Kitaalam bado haijulikani ni nini hasa kinachopelekea mabadiliko haya kwenye chembe hai hizi na hivyo kuvuruga utaratibu wake wa kuzaliana, na hivyo kupelekea kutokea kwa saratani. Hata hivyo madaktari wanatambua vitu ambavyo ni hatarishi na ambavyo vinaweza kuchangia kusababisha mabadiliko kwenye chembe hai hizi na hivyo kupelekea saratani.

SABABU HATARISHI

Zifuatazo ni mojawapo ya sababu hatarishi kwa kusababisha saratani kinywani:

  • Matumizi yeyote ya tumbaku kama vile sigara, ugoro nk
  • Matumizi ya vileo
  • Midomo kupigwa na jua kwa muda mrefu
  • Kupata maambukizi ya virusi kinywani
  • Kuwa na kinga dhafu

NAMNA YA KUJUA UGONJWA HUU

Saratani ya kinywa huweza kujulikana kitaalam baada ya kufanya uchunguzi kwa namna mbalimbali ikiwemo zifuatazo:

  • Uchunguzi wa kawaida. Daktari wa kawaida ama wa kinywa na meno anaweza kuangalia kinywani ili kuona kitu ambacho umemuelezea ili kujua kitaalamu ni nini.
  • Kufanya Uchunguzi wa kimaabara. Kama itaonekana ni kitu ambacho kinahitaji uchunguzi zaidi inaweza kushauriwa kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo sehemu ndogo ya eneo huchukuliwa kitaalam na kupelekwa maabara kwa uchunguzi zaidi. 

MATIBABU

Matibabu ya saratani hutegemea mahali hiyo saratani ilipo na iko kwenye hatua gani katika kuendelea kwako kushambulia mwili, hali ya jumla ya kiafya ya muhusika na pia mapendekezo ya mtu binafsi. Hivyo basi inawezekana kabisa ukawa na matibabu ya mara moja ama ukawa na mchanganyiko wa matibabu kulingana na vigezo nilivyovitaja hapo juu. Matibabu ya saratani yamegawanyika katika makundi yafuatayo

  • Upasuaji
  • Mionzi
  • Madawa

Hivyo ni vizuri kujadiliana na daktari ama jopo la madaktari wanaomtibu mgonjwa wa saratani ili kueleweshana na kukubaliana juu ya matibabu ya mgonjwa. 

UPASUAJI

Matibabu ya upasuaji kwenye saratani ya kinywa umegawanyika katika makundi yafuatayo;

  • Upasuaji kuondoa uvimbe. Katika upasuaji huu daktari anaweza kukata uvimbe wote na baadhi ya sehemu ambazo hazijafikiwa na uvimbe bado ili kujiridhisha kwamba chembe hai zote zenye saratani zimeondolewa. Saratani ambazo ni ndogo huweza kuondolewa kwa upasuaji mdogo, wakati saratani kubwa huhitaji upasuaji mkubwa zaidi, ambapo huweza kuhusisha hata sehemu za mfupa wa taya ama ulimi nk.
  • Upasuaji wa kuondoa saratani liyosambaa mpaka shingoni. Inapothibitika kuwa saratani iliyoanzia kinywani imesambaa mpaka kwenye maeneo ya shingo, ukubwa wa eneo la upasuaji huongezeka na kufikia maeneo ya shingo ili kuhakikisha kwamba sehemu zote zilizoathiriwa na saratani zinaondolewa na hivyo kuondoa uwezekano wa saratani kubaki na kisha kuanza tena kukua.

Upasuaji kwenye maeneo ya kinywa huweza kuathiri namna unavyoonekana na hata wakati mwingine hata uwezo wako wa kuongea, kula na kumeza chakula huweza kuathirika.

MATIBABU YA MIONZI

Mionzi hutumika kuua chembe hai ambazo zina saratani, matibabu ya mionzi pekee hutumika pale tu inapothibitika kuwa saratani yako iko kwenye hatua za awali. Halikadhalika mionzi huweza kutumika kama nyongeza baada ya upasuaji. Pia wakati mwingine mionzi huweza kuunganishwa na madawa anayopewa mgonjwa.

MADHARA YA MIONZI

Madhara yatokanayo na mionzi ni pamoja na yafuatayo kinywa kuwa kikavu, meno kuoza, kuharibika kwa mfupa wa taya, kutokea kwa vidonda kinywani, fizi kutoa damu, ngozi kuwa nyekundu kama iliyoungua.

Hivyo daktari ama jopo la madaktari wanaomtibu mgonjwa wa saratani ya kinywa hushauri mgonjwa kumuona daktari wa kinywa na meno kama ya kuanza matibabu ya mionzi ili kujiridhisha kwamba afya yako ya kinywa iko vizuri na kama kuna matibabu basi yaanze kufanyika kwanza kabla ya kuanza kwa mionzi

MATIBABU YA MADAWA

Haya ni madawa ambayo hutumika kuua chembe hai zilizo na saratani mwilini. Madawa haya huweza kutumika peke yake ama yakiwa yameunganishwa na matibabu mengine kama vile mionzi. Kwa kua mara nyingi madawa haya huongeza ufanisi wa mionzi, hivyo mara nyingi huunganishwa pamoja.

MADHARA YATOKANAYO NA MIONZI

Madhara yatokanayo na matumizi ya madawa haya kwenye matibabu ya saratani hutofautiana kutegemea na aina ya dawa unayotumia. Hata hivyo madhara ambayo mara nyingi huwapata Watumiaji wa madawa haya ni Kichefuchefu, kutapika na kunyonyoka kwa nywele.


Maoni, maswali na Ushauri fika Hospitali iliyo jirani upate ufafanuzi zaidi

read more
Meno Kulegea na Kung’oka Yenyewe

Meno Kulegea Na Hata Kung’oka Yenyewe

(Periodontitis)

Ni watu wengi hasa wa kuanzia umri wa kati na kuendelea hupatwa na hali hii ya kuwa na meno yanayolegea na wanapoyachunguza hukuta meno husika hayana matundu na hali hii ya meno kulegea haiambatani na maumivu yeyote kwenye meno husika  ama kinywani kwa ujumla wake. Kwa makundi mengine meno haya yaliyolegea huweza pia kung’oka kirahisi wanapong’atia kitu. Huu ni ugonjwa unaoathiri mfupa wa taya lililoshikilia meno husika, hivyo basi sehemu husika za mfupa wa taya ambazo hushikilia meno zinazoshambulia na ugonjwa huu huwa dhaifu na kipenyo chake kutanuka, mara kipenyo chake ambamo jino hujishika kinapotanuka jino husika huweza kulegea, kitaalamu ugonjwa huu huitwa Periodontitis.

Dalili Za Ugonjwa Huu

Zifuatazo ni baadhi ya dalili za ugonjwa huu, zingatia kwamba si lazima mtu mmoja awe na dalili zote hizi:

  • Fizi kujivuta kutoka kwenye meno na hivyo kuyafanya meno yaonekane ni marefu kuliko kawaida yake kabla ya ugonjwa huu
  • Meno kuachana na kutengeneza nafasi mpya katika meno yako ambazo hazikuwepo hapo kabla( mianya ya ukubwani)
  • Kutoka usaha kati ya meno yako na fizi
  • Meno yaliyolegea
  • Mabadiliko ya mpangilio wako wa meno

Ni Lini Umuone Daktari wa Kinywa Na Meno

Fizi zilizo na afya njema huwa ni ngumu zinapobonyezwa na pia zina rangi ya pinki iliyopauka. Hivyo kama fizi zako ni nyekundu, zinabonyea na kutoa damu kiurahisi, ama una moja ama zaidi ya dalili zilizotajwa hapo juu za ugonjwa huu, ni vema ukamuona daktari mapema. Kadiri unavyochukua uamuzi wa kumuona daktari mapema ndivyo unavyokua na nafasi nzuri zaidi ya kurekebisha uharibifu unaosababishwa na ugonjwa huu, halikadhalika kuzuia magonjwa mengine ambayo huweza kutokea kutokana na kuwepo kwa ugonjwa huu wa fizi uliokamaa (Periodontitis).

Sababu Za Ugonjwa Huu

Kwa watu wengi wanapojichunguza meno yao huona kuna tabaka fulani gumu ambalo huwa limejijenga kwenye meno yao katika eneo ambalo jino hukutana na ufizi, kwa meno ya chini mara nyingi huwa ni kwa ndani ambapo meno hutazamana na ulimi lakini kwa meno ya juu tabaka hili gumu huweza kutokea pande zote. Kitaalamu tabaka hili gumu huitwa ugaga na huwa haiwezekani uwezi kuondoa ugaga kwa kupiga mswaki ama kwa kufanya flosi badala yake unahitajika kufanyiwa usafi kitaalam ili kuundoa.

Kadiri tabaka laini na ugaga vinapokaa kwa muda mrefu kwenye meno yako, ndivyo hivyo huweza kuleta madhara. Mwanzoni huweza tu kufanya fizi zivimbe na kutoa damu unapopiga mswaki. Mwendelezo wa fizi kuvimba hupelekea kutengeneza kwa nafasi katika meno yako (pockets) ambazo pia hukaliwa na bakteria, tabaka laini na ugaga. Kadiri bakteria hawa wanapoendelea kuishi kwenye sehemu husika hutoa sumu (endotoxin) ambayo huhusika moja kwa moja na kuendelea kwa ugonjwa huu. Kadiri muda unavyokwenda ndivyo nafasi hizi huzidi kukua na kufika mfupa ulioshikilia jino ambao nao unaposhambuliwa huwa dhaifu na kushindwa kuendelea kushikilia jino ambalo baadae hulegea na hata kung’oka.

Sababu Hatarishi

Zifuatazo ni sababu ambazo uwepo wake kwa mtu huongeza uwezekano wa mtu husika kupata ugonjwa huu:

  1. Tabia za usafi wa kinywa zisizoridhisha
  2. Matumizi ya tumbaku
  3. Kisukari
  4. Uzee
  5. Kupungua  kwa kinga ya mwili kunakotokana na sababu mbalimbali kama vile VVU/Ukimwi nk

Madhara Zaidi (Complications)

Baadhi ya madhara ya ugonjwa huu ni yafuatayo:

  1. Kupoteza meno
  2. Kutokea kwa jipu na maumivu makali

Matibabu

Matibabu ya ugonjwa huu hulenga kusafisha meno na maeneo yanayozunguka meno pamoja na nafasi zilizojitengeneza (Pockets), ili kuondoa ugaga. Usafi huu hufanywa na daktari kwa vifaa maalumu hospitalini. Unapofanyiwa matibabu haya una nafasi nzuri ya kupona kama tu utazingatia namna bora ya kuhakikisha unafanya usafi wa kinywa vizuri na hivyo kuhakikisha kinywa na kisafi muda wote.

Mitindo ya maisha na matibabu binafsi

  • Fanya yafuatayo ili kujiepusha na ugonjwa huu:
  1. Fanya usafi wa kinywa kama inavyoshauriwa na daktari wako.
  2. Tumia mswaki ambao unaubadilisha kila baada ya miezi mitatu.
  3. Hakikisha unapiga mswaki mara mbili kwa siku asubuhi baada ya kula na usiku kbla ya kulala.
  4. Fanya flosi kila siku.
  5. Tumia dawa za kusukutua ili kusaidia kupunguza tabaka laini kwenye meno yako.

Kuzuia

  • Namna bora zaidi ya kuzuia ugonjwa huu ni kuanza kufanya na kufuatisha masharti ya usafi wa kinywa mapema kabisa katika maisha yako na kutoacha kamwe maishani mwako. Hii ikiwa na maana kupiga mswaki mara mbili kwa siku asubuhi na jioni na kufanya flosi mara moja kwa siku.
  • Muone daktari wa kinywa na meno mara kwa mara, na hasa mara moja kila baada ya miezi sita. Hata hivyo kama daktari wako ataona uko kwenye mazingira hatarishi zaidi anaweza kukupangia utaratibu wa kumuona mara nyingi zaidi

Maoni, Maswali na Ushauri: Fika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Kitengo cha Afya ya Kinywa na Meno upate majibu sahihi kwa Afya Yako

read more
Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.