FAMILIA YA HAYATI DKT. JOHN P. MAGUFULI, UVCCM WAUNGANA NA WAGONJWA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO (CZRH) KUENZI JUHUDI ZAKE ZA UANZISHWAJI WA HOSPITALI HII.

Posted on: March 16th, 2025



Katika kuelekea siku ya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John P. Magufuli, Machi 17, 2025, wananchi, viongozi na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) wameungana na familia kwenye matembezi ya amani kuenzi juhudi zake wakati wa uhai wake.

Katika matembezi haya yaliyo ratibiwa na familia kwa kushirikiana na Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) yamewahusisha watu mbalimbali ikiwemo baadhi ya viongozi wa serikali,wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo ambao wamefika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) na kutoa mkono wa pole kwa wagonjwa waliolazwa kama sehemu ya matendo ya huruma kwa wahitaji.

Akizungumza kwa niaba ya familia ya Hayati Dkt. John P. Magufuli, mtoto wa marehemu, Jesca John Magufuli, amesema familia hiyo inaungana na watanzania wote kuelekea kumbukizi ya kifo cha mzazi wao kwa kufanya matendo ya huruma kwa wagonjwa.

Amempongeza Rais @samia_suluhu_hassan kwa jitihada zake za kuendeleza mema yote yaliyoachwa na mtangulizi wake aliyekuwa Rais wa awamu ya tano ambapo, Hospitali ya rufaa ya kanda ya chato ni moja ya mradi ambao Mhe. Rais aliahidi kuuendeleza toka kwa mtangulizi wake na sasa hospitali hii imekuwa mkombozi wa wananchi wa Mkoa wa Geita na Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hii, wameishukuru familia pamoja na wananchi wote waliofika kuwajulia hali na kushukuru kwa kuwashika mkono.

Bi. Angelina Isac ni mmoja wa wagonjwa waliopata fursa ya kupewa mkono wa pole na familia na ameshukuru kwa huduma anayoendelea kupatiwa na wataalamu wa hospitali hii ambapo yeye na familia yake wameamua kuwapa watoto wao mapacha waliowapata katika hospitali hii majina ya John na Jesca ikiwa ni kuenzi mchango mkubwa wa Hayati Rais John P. Magufuli.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.