WANANCHI WAENDELEA KUPATA HUDUMA ZA UCHUNGUZI NA MATIBABU YA MAGONJWA YA MOYO YANATOLEWA NA WATAALAMU KLINIKI YA MOYO YA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO NA TAASISI YA MOYO JAKAYA KIWETE.
Posted on: October 7th, 2024Wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi wameendelea kunufaika na huduma za kibingwa na ubingwa bobezi za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bure katika maonesho ya saba ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Bomba mbili mjini Geita.
Huduma hizi zinatolewa na madaktari bingwa na bobezi wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wakishirikiana na madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH), lengo ni kuwasogezea huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo bure wananchi wa mkoa wa Geita, mikoa ya jirani na wageni kutoka nje ya nchi wanaofika katika maonesho haya.
Adam S. Adam mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, ni mmoja wa wanufaika wa huduma hizi za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.Ameishukuru Serikali kwa uwekezaji iliyofanya kwa kununua vifaa na mashine za kisasa na kuwawezesha wataalamu kutumia mashine hizi kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo ambayo sasa yamekuwa tishio kwa maisha ya wananchi.
“Nashukuru kwa huduma hii niliyoipata hapa, nimefanyiwa kipimo cha ECHO na kipimo cha umeme wa moyo bure bila kuchangia chochote tofauti kama ningeenda hospitali kufanyiwa uchunguzi pamoja na gharama za kufanyiwa vipimo hivi kuwa juu.Hii ni fursa kwetu sisi wananchi hata kama hatuumwi ni vyema kufanyiwa uchunguzi ili kujua hali ya afya ya moyo.Nimefanyiwa uchunguzi niko salama na daktari amenishauri kuendelea kuzingatia ulaji salama na kufanya mazoezi ili kujilinda na magonjwa ya moyo”
Huduma hizi za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zinatolewa na wataalamu na madaktari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) hadi ifikapo Oktoba 13, 2024.
Wananchi wote tunakaribishwa kusogea katika viwanja hivi ili kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo zinazotolewa bure.