WANANCHI WA WILAYA YA MBOGWE WAJITOKEZA KAMBI YA UCHUNGUZI NA MATIBABU KATIKA KITUO CHA AFYA MASUMBWE.*
Posted on: April 15th, 2025Wananchi wa Masumbwe na maeneo jirani wamejitokeza katika kambi maalumu ya siku tano ya upimaji na matibabu ya kibingwa kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Hospitali ya Rufaa ya kanda Chato (CZRH) inayoendelea katika Kituo cha Afya Masumbwe kilichopo Wilaya ya Mbogwe, Mkoa wa Geita
Upimaji na matibabu haya ya siku tano yanatolewa na Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa kushirikiana na Madaktari na Wataalamu wa Kituo cha Afya cha Masumbwe.
Ikiwa ni siku ya pili tangu kuanza kwa huduma hizi za kibingwa, zaidi ya Wananchi 178 wamefanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya Watoto, magonjwa ya upasuaji, magonjwa ya ndani, huduma za usingizi na ganzi salama pamoja na magonjwa ya macho.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato , Daktari Bingwa wa magonjwa ya akina mama na uzazi Dkt. Oswald Lyapa amesema, “leo ni siku ya pili tangu kuanza kwa upimaji huu na tayari tumeona wanawake 64 wanaume 53 na watoto 61.
Dkt. Lyapa amesema lengo la kufika katika hospitali hii ni kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa karibu yao ili kuwapunguzia muda na gharama wanazozitumia kufuata matibabu haya mbali na maeneo yao, lakini pia kuwapa ujuzi Madaktari wenzetu waliopo katika vituo vya afya ngazi za chini ili wapate uelewa zaidi na ujuzi wa kuweza kuwatibu wagonjwa wetu kitaalamu pindi wanapohitaji huduma za matibabu hasa za dharula na kitaalamu kuweza kuokoa Maisha yao.
“Kati ya wagonjwa tuliowaona wapo wanaohitaji uangalizi zaidi na tayari tumewapa rufaa ya kufika katika hospitali yetu ambao matatizo yao yanahitaji vipimo vikubwa vinavyopatikana katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato iliyopo kanda ya ziwa, na kwakuwa tayari tunao ushirikiano na kituo hiki basi wengine watakuwa chini ya uangalizi hapa na tutashirikiana na wataalamu katika kituo hiki kuhakikisha tunafuatilia maendeleo yao ya afya waweze kupona na kurudi katika majukumu yao”.
