GLOBAL MEDICARE KUSHIRIKIANA NA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO KUBORESHA NA KUWASOGEZEA WANANCHI KANDA YA ZIWA NA NCHI JIRANI HUDUMA ZA AFYA ZA KIBINGWA NA UBINGWA BOBEZI
Posted on: July 29th, 2025Chato,Geita
Julai 29, 2025.
Global Medicare imefanya mazungumzo na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kwa lengo la kushirikiana kuboresha na kuwasogezea wananchi wa kanda ya ziwa na nchi jirani huduma za afya za kibingwa na ubingwa bobezi.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Meneja Mkuu wa Global Medicare Bw. Daniel Lazaro amesema, “Lengo la kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) ni kuboresha ushirikiano kwa wataalamu, kujengeana uwezo na kuwa tayari kuungana na wataalamu wengine kutoka maeneo mbalimbali kutoa huduma za kibingwa kwa wananchi wote hasa ambao hawana uwezo wa kuzifuata huduma hizi za afya nje ya maeneo yao ya makazi na kanda ya ziwa”.
Naye Dkt. Oswald Lyapa kwa niaba ya Mkurugenzi wa Hopsitali ya Rufaa ya Kanda Chato, ameishukuru timu hiyo kwa kuchagua kuanza ushirikiano na CZRH katika kuwasogezea wananchi huduma za kibingwa na ubingwa bobezi na kuahidi kuwapa ushirikiano na hospitali ipo tayari kushirikiana nao kuwapa huduma za afya wananchi ambazo hapo awali iliwalazimu kuzifuata mbali na hata nje ya nchi.
