MWENYEKITI WA JUMUIYA YA WAZAZI TAIFA ATEMBELEA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO
Posted on: March 14th, 2024Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi taifa Ndugu Fadhili Maganya, leo 14 Machi 2024 ametembelea Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) kukagua miradi ya maendeleo ya utoaji huduma za afya ambapo amewataka watumishi wa afya kutoa huduma kwa uadilifu na kufuata kanuni za afya ili kuokoa maisha ya wananchi wanaofika hospitalini kupata huduma.
Bwana Maganya amezungumza haya mara baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya utoaji huduma iliyosomwa na Dkt.Oswald Lyapa ambaye ameeleza hali ya utoaji huduma kuimarika ukilinganisha na hali ilivyokuwa hapo mwanzo.
Dkt.Oswald amesema kuwa, uongezekaji wa huduma kama huduma za mifupa, uanzishwaji wa huduma ya kuchuja na kusafisha damu (Dialysis), huduma za kufua na kutengeneza hewa tiba (Oxygen), huduma za kliniki ya magonjwa ya moyo, kliniki za magonjwa ya masikio, pua na koo, uchunguzi wa kibingwa na bingwa bobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na mfumo wa hewa, huduma za kibingwa za uchunguzi kwa kutumia mashine ya MRI na CT Scan, zimekuwa chanzo cha uimarikaji wa huduma za afya na kuwapunguzia wananchi gharama za kusafiri mbali kufuata huduma hizi.
Dkt Oswald amesema kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya awamu ya sita ndani ya hospitali hii, pindi miradi inayoendelea kutekelezwa ikimalizika, ambayo ni jengo la ufuaji (laundry), jengo la kuhifadhia maiti( mortuary), jengo la kutakasia vifaa tiba, jengo la kusubiri wagonjwa pamoja na jengo la kulaza wagonjwa, huduma za afya katika hospitali zitaimarika zaidi na kusaidia wananchi kupata huduma zote hapahapa hospitali bila kuingia gharama za kusafiri kwenda mbali.