UMOJA WA VIJANA WA CHAMA CHA MAPINDUZI (UVCCM) WILAYA YA CHATO WAIPONGEZA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO KWA HUDUMA BORA NA LUGHA ZA STAHA KWA WANANCHI.
Posted on: May 10th, 2024Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Chato Cde. Pamphil James Hwago, leo Mei 10, 2024 amewaongoza vijana wa chama hicho katika ziara ndani ya hospitali ya rufaa ya kanda chato (CZRH) ambao wametembelea maeneo mbalimbali na kujionea hali ya utoaji huduma pamoja na kukabidhi cheti cha pongezi kutoka kwa umoja huo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi cheti hicho, Cde. Hwago ameushukuru uongozi kwa kuendelea kuhakikisha huduma zinaboreshwa na umoja huo wa vijana wamekuwa wakipokea sifa nzuri kutoka kwa wananchi ikiwa ni pamoja na lugha nzuri na zenye staha kwa wagonjwa waliofika hospitalini kupata huduma.
Cde. Hwago wakati akikagua utoaji huduma amesema, “Tumepokea pongezi nyingi kutoka kwa wananchi juu ya hospitali hii jinsi mnavyotoa huduma na kuwapa kipaumbele kwa kauli za staha kwa wagonjwa na hii imetufanya tutoe pongezi kwenu kwa mchango wenu kwa wananchi. Mnafanya kazi nzuri sana endeleeni kuwahudumia wananchi vizuri”.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato, Dkt. Oswald Lyapa ameushukuru Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) kwa kutambua mchango wa hospitali kwa jamii na kuahidi kuendelea kuboresha zaidi kwani serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt Samiah Suluhu Hassan inaendelea kuonesha ushirikiano kwa kuleta vifaa vya kisasa ambavyo hapo awali ilikuwa ni vigumu kuvikuta katika hospitali zilizopo kanda ya ziwa na sasa vinapatikana ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato hivyo kupunguza usumbufu kwa wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma. Lakini pia serikali imeendelea kuleta watumishi wa kada mbalimbali za afya ambao wamekuwa chachu ya maendeleo ya hospitali pamoja na uboreshaji huduma. Tutaendelea kuhakikisha tunalinda rasilimali hizi kwa manufaa ya wananchi wa Kanda ya Ziwa.