WANANCHI WA MKOA WA GEITA NA KANDA YA ZIWA WANUFAIKA NA MATIBABU YA KIBINGWA YA MAGONJWA YA MOYO YANAYOFANYIKA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO (CZRH).

Posted on: February 22nd, 2024

Zaidi ya wananchi 300 wamejitokeza kufanya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu katika kliniki maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa haya inayofanyika kuanzia tarehe 19 Februari, 2024 hadi ifikapo 23 Februari 2024.Kliniki hii inafanywa na madaktari bingwa bobezi kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH).

Kliniki hii maalumu ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu inalenga kuwafikia wananchi wa mikoa ya kanda ya ziwa ambao hapo awali walilazimika kufunga safari kwenda mbali kutafuta huduma hizi hali inayowafanya wengine kukata tamaa ya matibabu pamoja na kuishi na maradhi ya moyo bila kupata matibabu.

Haya yamebainishwa na Daktari bingwa bobezi wa magonjwa ya moyo na upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dkt.Emmanuel Ramadhani ambaye amesema;
"Dhumuni la kambi hii ilikuwa siyo kufanya upasuaji bali kuwabaini kwanza wenye matatizo ya magonjwa moyo na ikiwezekana kama ni wengi tuweze kuja na wataalamu na vifaa vya kutosha kwani hapa vyumba vya upasuaji vipo na vifaa vya kisasa. Katika wale waliobainika kuwa wagonjwa siyo wote wanahitaji upasuaji, wengine wanahitaji matibabu ya kutumia dawa kwa muda mrefu na uangalizi wa karibu hivyo watakuwa wakitibiwa na madaktari wa hapa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) ambao wapo na wamesomea magonjwa ya moyo hadi pale tutakaporudi kwani huduma hizi ni endelevu”

Naye mkurugenzi wa huduma za afya katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Dkt. Oswald Lyapa ameongeza na kusema, “Ushirikiano baina yetu na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kuanzia sasa unaenda kuokoa maisha ya watanzania wengi hasa wanaoishi kanda ya ziwa kwani wengi tumewapoteza kwasababu ya gharama hasa nauli na malazi kuwa juu na sasa huduma hizi zinapatikana hapa katika mkoa wa Geita, hivyo nipende kuchukua fursa hii kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuiendeleza hospitali hii kama ilivyopangwa kuwa na sasa huduma hizi zinaimalika

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.