WATUMISHI WA HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA CHATO (CZRH) WASHIRIKI KATIKA MAADHIMISHO YA SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI WILAYANI MBOGWE.

Posted on: May 1st, 2024

 Ikiwa ni Mei 1, 2024 Maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani yaliyofanyika Kimkoa katika Tarafa ya Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe iliyopo mkoa wa Geita, Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato CZRH) wameungana na watumishi wengine kutoka sehemu mbalimbali katika mkoa wa Geita kuadhimisha siku ya Wafanyakazi duniani. Kwa mwaka huu, 2024 kauli mbiu ya Maadhimisho haya inasema “Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha”.

Sherehe za maadhimisho haya zimeongozwa na Mhe. Martin Shigela, Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye ametumia maadhimisho haya kuhimiza utendaji kazi wenye kuleta matokeo chanya pamoja na kufanya kazi katika kuwahudumia wananchi kwa bidii na uadilifu.

Mhe. Shigela ameendelea kusema kuwa; Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan inathamini mchango wa wafanyakazi na ndani ya miaka mitatu aliyokaa madarakani mkoa wa Geita umepata zaidi ya watumishi elfu thelathini (30,000), huku akitolea mfano wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ambayo ilianza kutoa huduma za afya ikiwa na watumishi wachache lakini hadi sasa Serikali inaendelea kuleta Watumishi wa Afya hali inayopelekea huduma kuendelea kuimarika kila siku na Wananchi sasa wameanza kunufaika na matunda ya uanzishwaji wa hospitali hii.

Mwisho, Mhe. Shigela ametumia maadhimisho haya kutoa pongezi kwa watumishi hodari katika utoaji wa huduma kwa wananchi ambapo kwa upande wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato Bw. Peter Tarimo kutoka Kurugenzi ya Uuguzi, Bw. Akee Mkulula kutoka Kurugenzi ya Tiba, Bw. Masaka Julius kutoka Kurugenzi ya Tiba Saidizi na Bi. Godliver Kikene kutoka Kurugenzi ya Utawala wametunukiwa hati za pongezi na fedha taslimu kama watumishi hodari kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato kwa mwaka 2024.

Copyright ©2022 CHATOZRH . All rights reserved.